Geita. Tunaweza kusema ni majanga ya elimu. Tunasema hivi maana ni kama hakuna lugha rahisi ya kuelezea hiki kinachoonekana katika shule mbili za msingi; Nyamarere na Bweya zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita au Geita Vijijini kama ambavyo wengi hupenda kutamka.
Wanafunzi katika shule zote mbili wanaishi katika
mazingira ya enzi za ujima kwani wengi wao wanasomea nje kutokana na
uhaba wa vyumba vya madarasa na baadhi yao chini ya miti ili kusaka
kivuli, wakati wale wanaopata fursa ya kuingia katika madarasa wanakalia
mawe kutokana na ukosefu wa maadawati.
Kuna nyakati ambazo wanafunzi wa madarasa mawili
au matatu wanalazimika kutumia chumba kimoja na hapo mwalimu akiingia,
huwafundisha walio wake kwa maana ya darasa husika na wale wa madarasa
mengine huwa watazamaji iwe kwa dakika arobaini au themanini za somo.
Shule ya Msingi Nyamarere yenye madarasa ya kwanza
mpaka sita, ina wanafunzi 742; wasichana 315 na wavulana 427 pamoja na
walimu 12. Shule hii ina madarasa mawili tu na ofisi moja ya mwalimu
mkuu ambayo pia hutumika kama maktaba na stoo.
Hii inamaanisha kuwa kwa idadi ya wanafunzi
waliopo, chumba kimoja cha darasa kinapaswa kukaliwana wastani wa
wanafunzi 371. Kwa upande wake, Shule ya Msingi Bweya yenye wanafunzi
401 ina vyumba vitatu, hivyo wastani wa wanafunzi katika darasa moja ni
134.
Niliwasili katika Shule ya Nyamarere muda wa saa
04:00 asubuhi na ilikuwa ni asubuhi tulivu huku anga likiwa limefunikwa
na mawingu yaliyoashiria kwamba huenda mvua ingenyesha siku hiyo.
Nilipokewa vyema na mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Neema Martine ambaye alinikimbilia baada ya kuniona.
Mwanafunzi huyo aliyeonyesha nidhamu ya hali ya
juu, aliniamkia kisha kunipokea mizigo yangu akiamini pengine kuwa mimi
ni mwalimu mpya.
Baada ya kusalimiana, Neema aliwaongoza wanafunzi
wenzake waliokuwa wameketi katika moja ya makundi mengi yaliyokuwa
katika eneo hilo la shule akisema: “Heshima kwa mwalimu toa.”
Wanafunzi walisimama na kupiga saluti wakisema kwa
pamoja: “Shikamaoo mwalimu”. Baada ya tukio hili waliketi na kuendelea
na kile ambacho walikuwa wakifanya, ambacho kwa wakati huo sikufahamu
kilikuwa ni kitu gani.
Kadiri nilivyokuwa nikiingia katika mazingira ya
shule hii ya Nyamarere nilianza kuhisi kwamba makundi kadhaa ya
wanafunzi niliowaona wakiwa wameketi nje, ni madarasa na walimu wao
walikuwa wakiendelea kufundisha.
Wapo waliokuwa wameketi sehemu za wazi, wengine
pembezoni mwa kuta za vyumba vya madarasa vilivyopo, wengine waliketi
chini ya miti mikubwa ya miembe na wengine walikuwa wakiendelea na
masomo katika boma la jengo ambalo halijaezekwa.