Mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huu wa Ebola, ni kwamba mwanzoni mataifa yaliyoathirika na hata jamii ya kimataifa ilipuuza uzito wa janga hili.
Ugonjwa wa Ebola ni kana kwamba ulikuwa “unaogelea katika bahari ya taifa lisilojali, kujidanganya, na lisilo na uwezo na ufahamu wa kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huu," anasema mtaalamu wa masuala ya virusi nchini Nigeria, Oyewale Tomori.
Kuna maswali mengi kuliko majibu. Mfano, nini kinachotokea mwilini baada ya mtu kuambukizwa Ebola? Je, vijana wananafasi nzuri ya kupambana na Ebola kuliko wazee? Miakia 40 kabla ya kuzuka kwa mripuko wa sasa, ni watu 2,500 pekee waliofariki kutokana na Ugonjwa wa Ebola, idadi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na watu wanaoambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi au kifua kikuu kila siku. Jamii ya kimataifa bado haijafaulu kupata njia bora za kupambana na ugonjwa huu wa Ebola.
Tangu kuzuka kwa ugonjwa huo katika mataifa ya Afrika Magharibi, juhudi za kupata dawa ya kuutibu zimeimarishwa kote duniani. Shirika la Afya Duniani (WHO) lina matumaini ya kutoa chanjo kwa maelfu ya watu wanaoishi katika mataifa yanayoathirika zaidi na ugonjwa huu kufikia katikati mwa mwaka 2015. Na kufikia mwishoni mwa mwaka huo wa 2015 shirika hilo linatarajia litakuwa limetoa chanjo kwa watu milioni moja dhidi ya ugonjwa huo.