Header ads

Header ads
» » SERA YA TAIFA YA MAENDELEO YA VIJANA HAINDANI NA WAKATI HUU

VIJANA ni nguvu kazi ya taifa kama inavyoaminika kwa kila nchi kutokana na kwamba asilimia kubwa ya uchumi unaozalishwa unatokana na nguvu ya vijana.
Kwa maana hiyo, vijana wanapopewa mwongozo mzuri juu ya kujiletea maendeleo ya kupambana na maadui maradhi, ujinga na umaskini sina shaka uchumi wetu utakua kwa asilimia kubwa.
Nasema hivi nikiwa na maana kwamba sera ya maendeleo ndio msingi na dira imara kwa kijana ambaye ana nguvu na uwezo wa kuzalisha na kuinua uchumi wa nchi yake.
Kinyume chake kutokuwa na sera na misingi imara kwa vijana, nikiwa na maana kwamba misingi ya kiutamaduni, kidini, kijamii na kielimu ni kikwazo kwenye uchumi wetu.
Kwa kawaida sera ya maendeleo kwa kijana lazima impe fursa kijana kujiamini, kujitambua na kuchangia maendeleo ya taifa, pia kutambua changamoto zilizoko ndani ya jamii na zile zilizo nje ya jamii yake.
Pia inapaswa kumpa kijana fursa ya kubainisha, kuainisha na kutumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa mfano, wimbi kubwa la vijana waliokosa ajira nchini inatokana na kukosekana kwa sera na misingi imara ya kumwezesha kijana kujiamini, kujitambua na kumpa uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla, sina shaka na maneno haya.
Changamoto ya uzao wa vijana usiofuata utamaduni wa nchi yao, usiofuata maandiko ya vitabu vya dini au miiko ya dini, usiofuata misingi na maadili ya jamii, usiofuata sheria, usiofanya kazi za kuinua uchumi wa taifa lao ni matokeo ya sera ya maendeleo kwa vijana kuwa na upungufu.
Uzao wa vijana legelege, vijana tegemezi wasiopenda kuchosha akili (kufikiri na kuona mbali) na kujishughulisha ili kujipatia kipato ni zao lililokosa sera na misingi ya maendeleo.
Kwa tafsiri tofauti, vijana wengi wamekosa uzalendo, wamekuwa legelege (wamekosa ukakamavu) wa kufanya kazi pia wamekosa uthubutu wa mawazo, fikra na hata maamuzi ya kufanya jambo lenye kuleta tija au maendeleo kwa taifa.
Hadi kufikia mwaka 1996 Tanzania haikuwa na sera ya maendeleo ya vijana iliyokamilika na kuwahamasisha vijana kujikwamua kwenye umaskini na kujiletea maendeleo.
Sera hii chini ya Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana ilikuwa na madhumuni ya kuboresha maisha ya vijana kwa kuwaendeleza katika nyanja za kiuchumi, utamaduni, siasa, malezi na elimu.
Hii ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua fursa za maendeleo zilizopo.
Pia ilikuwa na lengo la kuhamasisha vijana na jamii katika kutambua, kukuza na kulinda haki za vijana kulingana na Katiba ya nchi.
Lengo lingine ni kushirikisha idara, taasissi na vyombo mbalimbali katika kutekeleza mipango ya kuwaendeleza vijana kwa lengo la kudhibiti athari mbaya zinazotokana na michakato ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Pia ilikuwa na lengo la kuwaandaa vijana kimwili, kiakili, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ili waweze kuchukua majukumu mbalimbali kama raia wema, wazazi na viongozi katika jamii pamoja na kuwawezesha vijana kushiriki katika juhudi za kuleta maendeleo ya jamii na taifa.
Kwa hiyo, kadiri miaka ilivyozidi kusogea mahitaji pamoja na mazingira ya vijana yanazidi kubadilika. Sera ya vijana ya mwaka 1996 ilionekana kuwa na upungufu kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, utandawazi, elimu na mabadiliko ya mfumo mzima wa maisha kwa vijana.
Mwaka 2007 Sera ya Taifa ya maendeleo ya vijana iliundwa upya lengo likiwa kuwaendeleza vijana na kujikwamua kwenye umaskini.
Kutokana na sera hii ya mwaka 2007 hivi sasa mwaka 2013 inaonekana bado kuna upungufu kutokana na mabadiliko hasa kwenye mfumo mzima wa maisha ya vijana.
Sera ya maendeleo ya vijana imeshindwa kumjengea uwezo kijana kujiamini na udhubutu kwenye masuala ya maendeleo.
Tanzania tumejiunga na nchi za ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kibiashara tukiwa na lengo la kunufaika na fursa za kibiashara kwenye nchi za hizo tukiamini tuna sera zinazomlinda kijana.
Pia sera hii ya maendeleo ya vijana tukitegemea itakuwa na mwamko wa kuwahamasisha vijana kujijengea uwezo wa kujiamini na kudhubutu kwenye fursa kama hizi ambazo kwa hakika bila sera imara hatuwezi kufika mbali kibiashara.
Utafiti wangu umebaini bado hatuna sera imara zinazoweza kushindana kwenye biashara hasa pale inapotokea tumejichanganya na nchi nyingine kwenye masuala ya maendeleo.
Kwa mfano, Tunawaona wenzetu wa Kenya na Uganda wanavyokuja juu kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kibiashara, Tanzania bado tunajikongoja.
Mwitikio wa kibiashara kwetu bado ni mdogo ukilinganisha na wenzetu wa Uganda na Kenya.
Hii inatokana na uwezo wa utambuzi wa kijana kwenye sera ya maendeleo ya mwaka 2007 ikiwa ni ya kinadharia kuliko kiutendaji.
Nakumbuka kabla ya sera ya mwaka 1995 kutumika vijana walikuwa wanahimizwa kufanya kazi za kujitolea kwa vitendo kwa mfano kulikuwa na miradi ya maendeleo iliyokuwa kwenye ngazi za kijamii ambayo vijana walihusishwa kufanya kazi za kujitolea kwenye mafunzo ya jeshi.
Hizi zilikuwa sera za ujamaa na kujitegemea, zilizokuwa zikitolewa kivitendo ambapo ziliwajenga vijana kujiamini na kuonesha udhubutu kwenye shughuli za kimaendeleo.
Mambo yanayofanyika hivi sasa ambapo wakati wa ujamaa na kujitegemea yalipingwa vikali kwenye sera ya ujamaa mfano, vijana kujihusisha kwenye vurugu zinazohatarisha amani ya nchi ni miongoni mwa sababu zilizomfanya kijana kuelewa na kuupigania uzalendo wa nchi yake.
Kuna masuala kama kijana kujihusisha kwenye rushwa, uhujumu uchumi, ubinafsi nakadhalika ni miongoni mwa mambo ambayo sera ya ujamaa na kujitegemea ilivipinga vikali tena kwa vitendo.
Kwahiyo, misingi ya kijana ilitokana na sera imara iliyokuwepo kwa wakati ule. Uzalendo ulionekana miongoni mwa vijana pale sera ya Ujamaa iliposema kwa dhati kutoka moyoni kwamba rushwa ni adui wa haki na viongozi wakaiheshimu.
Kujiamini kwa kijana na kuthubutu kwa maslahi ya nchi yake vilionekana kwa kujitolea hata bila kulipwa mshahara. Ni ishara inayoonesha kwamba vijana walitambua misingi yao kama vijana pia sera imara yenye kuendana na wakati uliokuwepo.
Sera ya maendeleo ya vijana itambue kwamba mfumo wa maisha ya vijana unatakiwa ubadilike na uendane na wakati; hasa ukizingatia dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto lukuki kama teknolojia, mabadiliko ya tabia ya nchi, uharibifu wa mazingira na dawa za kulevya.
Ni wajibu wa wizara husika kuziangalia sera hizi ili kijana aendane na wakati na mfumo wa changamoto wa kidunia.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post