![]() |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ZAIDI
YA WANAWAKE 600 KUNUFAISHWA NA ELIMU YA UJASILIAMALI MKOANI MWANZA.
Wanawake
mkoani Mwanza, wanatarajiwa kupata elimu juu ya ujasiliamali na fursa zilizopo,
Usimamizi wa fedha na uwekaji akiba pamoja na mafunzo ya afya bora kama kiini
cha uchumi imara kupitia kampeni kubwa ya Mwanamke na Uchumi itakayofanyika
katika viwanja vya Mwaloni jijini Mwanza kuanzia tarehe 4 na 5, Septemba, 2014 ambapo
akina mama na vijana zaidi ya 600 kutoka wilaya za Magu, Ilemela, Misungwi na
Nyamagana zitashiriki kikamilifu katika kampeni hii itakayotolewa na taasisi ya
ANGELS MOMENTS ya jijini Dar es salaam ambapo akina mama na vijana zaidi ya 600
watashiriki kikamilifu.
Kampeni
hii inayolenga kutoa elimu ya msingi na shirikishi inalenga kuwajengea uwezo na
ujuzi wa kusimamia fedha zao kwa lengo la kunyanyua uwezo wao wa kiuchumi
pamoja na familia zao, kampeni itahusisha semina zitakazotolewa na wakufunzi
mahiri katika Nyanja za uchumi, fedha na utambuzi wa fursa.
Kampeni
hii ambayo ni ya pekee na ya aina yake hapa nchini imeanzia mkoani Mwanza kwa
kutambua fursa zilizopo mkoani hapa hivyo wanawake wa mkoa huu watapewa elimu
ya msingi ya kibiashara na kuchochea uelewa wa wanawake hawa katika
kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo ndani na nje ya mkoa wa Mwanza.
Kwa
kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na taasisi ya WAMA
tunatarajia kuwafikia wanawake wa vikundi vyote vya kijamii, SACCOS, AMCOS,
VICOBA na makundi mengine Ya kijamii yanayojihusisha na wajasiriamali na hivyo
kampeni hii itawawezesha kujiongezea uwezo wa kupata wateja wa bidhaa na huduma
zao na kujitangaza zaidi.
Wanawake
wengi kama mnavyojua wamekuwa wahanga wa kukumbwa na kadhia ya madeni na
kukatiza biashara zao na wengine kuogopa kufanya biashara na ujasiriamali kwa
sababu ya ama kukosa elimu au kukumbwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na
ama kununua vitu kama vipodozi, viatu na vitu vingine kwa kuharibu mtaji wake
na wamejikuta hawana msemaji na mtu wa kuwaelimisha na kuwasaidia.
ANGELS
MOMENT kupitia kampeni hii ya mwanamke na uchumi inakuja kuwa jibu la
changamoto tajwa za wanawake na wajasiliamali kwani tunatilia mkazo elimu juu
ya bajeti, ukokotoaji wa kodi, elimu juu ya tabia za matumizi chanya na ulipaji
madeni na mikopo.
Pamoja
na mkoa wa Mwanza kampeni ya Mwanamke na Uchumi pia itafanyika katika mikoa ya
Tanga, Kigoma, Dodoma, Pwani, Ruvuma na Lindi kuanzia mwishoni na mwanzoni mwa
miezi ya septemba hadi Januari 2015 mtawalia.
Kampeni
hii itaambatana na burudani kutoka kwa balozi wa wanawake ambae ni mwanamuziki
LINAH SANGA. Pia kutakuwa na michezo ya kuigiza pamoja na filamu zinazoelimisha
wanawake wajasiriamali na kuwapa ujasiri wa kujikomboa.
Tunawaomba
wanawake wote watakaopata fursa hii waitumie ipasavyo ili elimu itakayo tolewa
ikawe ni chachu ya mabadiliko kwa familia nzima na Taifa kwa ujumla wake, kwani
tunaamini katika kauli mbiu yetu “ UKIMUELIMISHA MWANAMKE UMEELIMISHA JAMII
NZIMA”
Hivyo
tunatarajia ndugu wanahabari mtusaidie kufikisha ujumbe huu kwa jamii nzima ya
Tanzania kwani maendeleo ya wanawake wa Tanzania ni Maendeleo ya Uchumi wa
Taifa letu.
-ASANTENI-
IMETOLEWA NA:
Mkurugenzi Mkuu
Angels
Moment Co. Ltd
DAR
ES SALAAM
Agosti
27, 2014
Afisa Uhusiano wa TBS Roida Andusamile, pamoja na Meneja wa Kanda ya ziwa wa PPF Bwana Meshach Bandawe wakifuatilia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mapema leo katika ukumbi wa Gold Crest kuwahabarisha kuhusu kampeni ya Mwanamke ya Uchumi itakayofanyika jijini Mwanza tarehe 4-5 Septemba, 2014 katika viwanja vya Mwaloni Kirumba Jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa Angels Moment akiongea na waandishi wa habari mapema leo katika ukumbi wa Gold Crest kuhusu Kampeni ya Mwanamke na Akiba inayotarajiwa kufanyika Mkoani Mwanza kwa siku mbili. Zaidi ya wanawake wajasiriamali 600 wanatarajiwa kufaidika na mafunzo haya yatakayotolewa bure jijini humo.
Afisa Uhusiano wa TBS Roida Andusamile akielezea jukumu la TBS katika kuwaelimisha wanawake wajasiriamali wa Kitanzania watakaoshiriki katika kampeni ya Mwanamke na Uchumi juu ya ubora na viwango katika bidhaa wanazoandaa.
Bi Roida wa TBS akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema leo.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza Bwana Hamis Fakii akielezea umuhimu wa akinamama kujiwekea akiba katika Mifuko ya Pensheni kwa Maisha yao ya sasa na ya baadae, Pia kujiunga na skimu ya SHIB ili wapate matibabu na familia zao kwa kuchangia pesa kidogo sana.
Bwana Lutufyo Mtafya ambae ni afisa huduma na elimu wa TRA Mkoa wa Mwanza akielezea umuhimu wa wanawake wajasiriamali wa kitanzania kutunza mahesabu yao kwa kutumia mashine za EFD.
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa PPF Bwana Meshach Bandawe akielezea kwa wanahabari jinsi PPF inavyosaidia wanawake wajasiriamali walio katika sekta isiyo rasmi kwa kuwapa mikopo kupitia SACCOS.
Mkurugenzi Mkuu wa Angels Moment akijibu maswali aliyoulizwa na wanahabari wakati wa Mkutano kuhusu Kampeni ya Mwanamke na Akiba itakayofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
