Muuguzi wa hospitali hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema walimpokea mtoto huyo kwa maelezo kuwa anaharisha. Lakini walipoona tatizo lake ni kubwa, waliwasiliana na daktari wa magonjwa ya watoto, Dk Omar Maiza ili kumfanyia uchunguzi zaidi.
Alisema baada ya daktari huyo kumchunguza kwa mara ya kwanza, ilionekana kuwa mtoto huyo alikuwa amelawitiwa zaidi ya mara moja. “Ilitushtua kuona mtoto akiingiziwa vidole sehemu ya haja kubwa na vikiingia bila shida. Huu ni ukatili mkubwa kwa watoto,” alibainisha muuguzi huyo.
Dk Maiza alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo hospitalini kwake, lakini akasema taarifa zaidi atazitoa leo. Mama wa mtoto huyo alifariki dunia mwezi mmoja tu baada ya kujifungua watoto pacha.
Hata hivyo, pacha mmoja wa kiume naye alifariki muda mfupi baadaye kwa maradhi kama hayo ya kuharisha.
Baada ya mama wa pacha hao kufariki, ilibidi baba wa watoto hao kutafuta mfanyakazi wa kushinda nao wakati yeye akiwa kazini.
Akizungumza na Mwandishi jana, mlezi wa mtoto aliyefanyiwa ukatili huo, Saada Ismail alisema waliamua kumpeleka mtoto huyo hospitali baada ya kuona anaharisha kuliko kawaida.
Alisema siku zilizopita alikuwa vizuri na yeye ndiye aliyekuwa akimbadilisha nguo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema hakuwa na taarifa za tukio hilo.