Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuanzia leo wametakiwa kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Majini na Nchi Kavu (Sumatra) pindi watakapotumia usafiri wa mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) yasiyokuwa na vibao vinavyoonyesha njia.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Ofisa
Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Kishio namna
walivyojipanga kudhibiti makosa ya ukiuwakwaji wa sheria za huduma za
usafiri wa umma zinazofanywa na baadhi ya madereva ya mabasi hayo.
Kishio alisema Sumatra imekuwa ikitoa adhabu
mbalimbali kwa madereva wa mabasi hayo ikiwa ni wiki mbili sasa zimepita
tangu ilipoyakamata mabasi zaidi ya 20 yaliyokutwa na makosa mbalimbali
ikiwamo kutokuwa na leseni ya kusafirishia abiria ya Sumatra, stika na
vibao vinavyoonyesha njia yapitazo.
“Tutaendelea kuyafuatilia pamoja na mabasi mengine
ya abiria lengo letu ni kutaka kila dereva anafuata sheria
zilizowekwa,” alisema Kishio.
Alisema wamekuwa wakiyatoza faini ya Sh 350,000
kwa kosa la kukatisha njia, lakini kwa kuwa jambo hilo linaonekana
kushamiri, wamepanga kuongeza kiwango cha faini hadi kufikia Sh 500,000.
Kishio aliwataka madereva wa Uda kutoondoa vibao
vinavyoonyesha njia na kusisitiza kuwa kila basi lililoomba kusafirisha
abiria lina wajibu wa kufika mpaka mwisho wa kituo kama ruti yake
inavyomuelekeza na kwenda kinyume na hapo ni kosa ambalo abiria
wanapaswa kulipigia kelele.