JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jana limelazimika kutumia mabomu ya machozi na kuwatia mbaroni waumini 29 wa Kanisa la Moravian Usharika wa Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kutokea vurugu za waumini kanisani hapo.
Akizungumza na Majira, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura, alikiri jeshi hilo kuwatia mbaroni waumini hao na kusema kuwa, taratibu zikikamilika watafikishwa mahakamani.
Hali ya kuvunjika kwa amani kanisani hapo, ilianza saa moja asubuhi ambapo pande mbili za waumini hao ambazo zimekuwa zikipingana muda mrefu, zilishindwa kuelewana na kusababisha vurugu ambazo ziliingiliwa kati na jeshi hilo.
Awali kulikuwa na habari kuwa, zaidi ya watu 30 walikuwa ndani ya kanisa hilo eneo la juu tangu juzi ambapo jana asubuhi, watu hao walipelekewa vyakula na waumini wenzao ambao hawakulala ndani ya kanisa hilo.
Wakati waumini hao wakianza kuingiza chakula ili kuwapelekea wenzao waliokuwa juu wakati eneo la chini wakiendelea na ibada, ndipo hali ilipoanza kuchafuka baada ya upande mmoja kuzuia chakula kisipelekwe kwa waumini waliokuwa juu ya kanisa hilo.
Polisi walifika eneo la tukio saa 1:40 wakiwa katika gari lenye namba za usajili PT 2118 ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni iliyoandikwa (OCD Kinondoni), ikiwa na askari ambao walipiga kambi nje ya kanisa hilo.
Askari hao hawakuingilia mzozo huo lakini waliwaonya waumini hao kuwa kama mmojawapo ataanza kumshika mwenzake na kusababisha vurugu basi watamkamata mara moja lakini ikiwa hawatagusana wao hawataingilia.
Waumini hao waliendelea kuzuiana ambapo vyakula vilivyoletwa kanisani hapo ambavyo ni chipsi, kuku, soda, maji na miswaki vilimwagwa na vyombo kutupwa nje ya eneo la kanisa hali iliyosababisha waumini hao kuanza kushikana ambapo wengine walitumia hadi mafagio ili kupigana.
Baada ya kuona hali hiyo Jeshi la Polisi lililazimika kuwakamata wale waliosababisha vurugu hali iliyosababisha askari mmoja kung’olewa vifungo vitatu vya shati lake wakati wa vurugu za kuwakamata.
Baadaye polisi waliamua kuwaachia waumini waliowakamata ambao ndio walioanza kuwagusa wenzao lakini waliwaachia na kuamua kuondoka eneo la kanisa wakiwa na gari lao.
Dakika chache baadaye, liliingia basi dogo likiwa na waumini zaidi ya 20 ambao inadaiwa walitokea katika Kanisa la Mabibo na kuanza kuimba ndipo hali ikachafuka ambapo polisi walirudi haraka kanisani hapo wakiwa wameongeza askari wengine, kupiga mabomu ya machozi na kuwatia mbaroni waumini hao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mchungaji wa Kanisa hilo, James Mwakalile, alisema anajisikia vibaya sana kuona mgogoro ukiendelea na wanaogombana ni walei si viongozi.
Alisema yeye anataka amani katika kanisa hilo na amejitahidi sana kuwaita upande wa pili ili wazungumze lakini hakuna lililofanyika.
Majirani waishio jirani na kanisa hilo, wamesema wamechoshwa na hali ya mgogoro unaoendelea kwani wanaoleta vurugu hizo wengi si wakazi wa hapo na kuitaka Serikali kulifunga kanisa hilo kabla mauaji hayajatokea.