Dodoma. Kama siyo kuzuiwa na mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana angezua tafrani bungeni kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Sakata hilo lilitokea jana asubuhi baada ya
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge hadi
jioni, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno
bungeni. Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi, akijibu
mapigo baada ya mbunge huyo kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Waliomzuia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose
Migiro, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George
Simbachawene na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk
Abdulla Juma Saadallah.
Mawaziri hao walimsindikiza Werema hadi nje ya Ukumbi wa Bunge na kutoweka.
Ilivyokuwa
Hali ilianza kuchafuka wakati Jaji Werema alipokuwa akijibu mwongozo uliombwa na Kafulila kuhusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mwongozo huo, Kafulila alisema Wizara ya
Nishati na Madini kupitia Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo
alizungumza uongo mara mbili bungeni kuhusiana na fedha za akaunti ya
Escrow.
“Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za
Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda
kinyume...” alisema.
Alisema katika hukumu hiyo ya Septemba mwaka jana,
hakuna mstari hata mmoja unaosema kuwa fedha za Escrow wapewe Kampuni
ya IPTL.
“Profesa Muhongo aliliambia Bunge kuwa Serikali
ililipa fedha hizo ili kuondokana na kesi hiyo lakini ninazo nyaraka za
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuteua kampuni mbili za uwakili
kwenda kuiwakilisha katika kesi nchini Uingereza,” alisema Kafulila.
Alisema kwamba aliomba mwongozo sababu huo umekuwa
mwendelezo wa kuzungumza uongo bungeni... “Naibu Waziri (Nishati na
Madini - Stephen Masele), alizungumza uongo bungeni tukaambiwa kuwa
wamekutana katika sherehe za kuzaliwa yakaisha, haiwezekani, Bunge ni
sehemu ya kuisimamia Serikali.