Rais
Jakaya Kikwete amesema mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta
matumaini kwa kupanua wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa na
kuiwajibisha Serikali.
Hata
hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze
kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo, ni lazima uendeshwe kwa watu
kufuata sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya nguvu, ambayo yanaweza
kuvuruga nchi.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,
aliyasema hayo juzi wakati alipotoa Mhadhara kuhusu Usalama wa Taifa
kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
Alikuwa
anajibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili kwenye chuo hicho kutoka
Kenya, ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya siasa, vinaathiri
umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi ya 30 ya
Tanzania, kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika
na Waafrika.
Rais Kikwete alisema:
“Vyama vingi ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini kwa
kupanua wigo wa kisiasa, ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma.
Sasa mtu anaweza kuamua kujiunga na chama chochote cha siasa
anachokipenda yeye.”
Aliongeza kusema: “Ni
mfumo ambao unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa
demokrasia. Sasa watu wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya safari za
Rais nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na
Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka zaidi kama Rais atabakia
amejifungia ndani ya nchi.”
Rais Kikwete alizidi kujibu swali hilo: “Jambo
la maana ni kwamba tunahitaji aina mbalimbali ya mawazo. Mawazo ya
namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo yanasaidia hata
chama changu kuimarika zaidi.”
Hata
hivyo, Rais Kikwete alisema mfumo huo, utavurugika, endapo baadhi ya
watu wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja za nguvu, badala ya
kupambana kwa hoja na nguvu ya hoja.
“Wasiwasi
wangu ni kuingiza matumizi ya nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni
makosa kwa watu kukimbilia kutumia nguvu baada ya kushindwa kwenye hoja.
Na hili halivumiliki na likitokea basi Serikali itaingilia kati
kudumisha amani,” alisema.