Makinda alisema hayo bungeni jana, alipokuwa akitoa muongozo ulioombwa
na Kafulila, aliyesema kuwa maisha yake yako hatarini baada ya Werema
kumtolea kauli zinazoashiria kumtishia maisha.
Katika maelezo yake, Kafulila ambaye alitaka wananchi wa jimbo lake
kufahamu lolote baya litakalomtokea litakuwa limesababishwa na Werema,
alisema pia amemwandikia Spika barua kuelezea hilo.
Hata hivyo Spika Makinda alijibu Kafulila kwamba anashangaa barua hiyo
hata kabla ya kuifungua, imeshatoka katika vyombo vya habari.
Alimtaka Kafulila kama ana ushahidi kuhusu suala la akaunti ya Escrow na
IPTL, apekekea kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na
Taasisi wa Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ambao
wanalishughulikia.
Spika alisema shinikizo analotaka kuchukua Kafulila katika suala hilo, linamfanya aone kwamba suala hilo si la kawaida.
Hivi karibuni Kafulila aliibua tuhuma bungeni akiwahusisha mawaziri
wawili pamoja na Sh bilioni 200 za Akaunti ya Escrow, iliyokuwa
inamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme(Tanesco) na Kampuni ya
kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited(IPTL).
Katika tuhuma hizo, alimuunganisha pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Maswi na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wa
Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Hata hivyo, suala hilo sasa limekabidhiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) ili kubaini ukweli wake.
Kutokana na suala hilo, wiki hii Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, aliteleza ulimi na kumwita Kafulila tumbili,kutokana
na kuendelea kulieleza jambo hilo bungeni.
Jaji Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Kafulila,
kuhusu fedha hizo ambazo alisema si za Serikali, kama inavyodaiwa na
Kafulila, kwa kuwa fedha za Serikali, hazikai katika akaunti hiyo.
Jaji Werema alisema kuna watu walileta bungeni vipeperushi, wakidai ni
ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha
na rushwa na Kafulila ndiye wanaoeneza uvumi huo. Wakati akizungumza,
Jaji Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole unaosema kwamba:
‘Tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni’. Kabla ya kufafanua maana ya
msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti, alikuwa akipiga kelele
kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa, hivyo atangaze maslahi yake.
“Naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Jaji Werema.
Kitendo hicho kilimkera Kafulila aliyeandika barua kwa Spika Anne
Makinda na hata Mwenyekiti wa bunge, Mussa Azzan Zungu alipotaka
kuwasuluhisha Kafulila alikataa.