Angalia jinsi maisha yanavyozidi kuwa magumu katika jamii zetu. Gharama za vyakula, usafiri, na mambo mengine zinazidi kuongezeka, pia mabadiliko ya kiteknolojia na kijamii yanaleta changamoto nyingi. Tupo katika zama ambapo kusimama kiuchumi kunahitaji kujidhatiti kweli kweli. Makala hii inachambua mambo ya msingi ambayo yanaweza kukusaidia kujipanga kupata dili zinazoweza kuinua maisha yako.
1. Jitafakari:
Ni vizuri kujizoesha kutafakari kuhusu wewe ni nani, mapungufu yako,
mambo gani makubwa na mazuri uliyokwisha wahi kufanya, na vitu gani hasa
unavipenda na usivyovipenda. Tafakari hii itakupa picha ya aina gani ya
mtu wewe ulivyo, na kukusaidia kujipanga kuziba yale mapungufu, na
wakati huo huo, utaweza kuangaza fursa zilizopo na unazoweza kuzitumia kutokana na 'ubora' ulionao.
Tafakari hii itakuwezesha pia kutambua kitu kiitwacho kwa kiingereza
'passion', yani mambo unayoyapendelea sana kufanya au kuwa hapo baadae.
Umuhimu wa kutambua passion ni kwamba ukiweza kuwekeza muda katika
passion yako inaweza kuwa sehemu nzuri ya kujijengea maisha yenye
furaha. Kwani passion itakufanya ufanye jambo utalotaka kulifanya kwa
ufanisi na pia hata ukikumbana na changamoto, hautokata tamaa kirahisi
rahisi.
2. Mambo mazuri hayataki haraka
Kumbuka hao wote unaowaona wamefanikiwa kimaisha, mafanikio ambayo
pengine unatamani uwe nayo, sio kwamba mafanikio hayo yalikuja kwa siku
moja. Kuna maandalizi kadhaa waliyafanya, magumu waliyoyapitia mpaka
kufika hapo walipofika.
Hii kwako ina maana kuwa ni lazima ujue kuna muda ni lazima uutumie
kufanya maandalizi, inabidi utambue kuwa utakutana na magumu, ila
hautakiwi kukata tamaa. Na zaidi sana ni lazima ujue bidii inahitajika.
Hata hivyo bidii zako zitazaa matunda kwa haraka kama utatambua
mapungufu yako mapema, na pia passion yako hasa ni ipi. Ukitambua
mapungufu yako mfano una tatizo la lugha ya kiingereza, basi utafanyia
kazi pungufu hilo ili uwe bora zaidi.
3.Utafiti ni muhimu sana
Ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi kuhusu nini vinaweza kufanikisha
mipango yako na matarajio yako ya kimaisha. Mfano kama unatamani
kufanya biashara, basi tafakari aina gani ya biashara, tafuta taarifa za
kutosha kuhusu wateja wa biashara husika, kiasi cha mtaji , mbinu za
kimasoko , n.k Vyote hivyo vitakuwezesha kujipanga kwa ufasaha ili
kupunguza hasara na muda mrefu wa kufikia mafanikio.
Hii pia inahusika katika aina ya kazi unayotamani kufanya, je ni kwa
kiwango gani utahitaji lugha ya kigeni, uwezo wa kutumia teknolojia
mpya, kiwango cha elimu , n.k
4.Kubali kuwa tofauti
Wewe na yule mna historia tofauti za maisha, malezi tofauti, tabia
tofauti, na hata uwezo wa kufikiri na hisia tofauti. Vyote hivi vinaweza
kuchangia katika namna tofauti za kukabiliana na changamoto za
kimaisha, na hata katika kupata fursa. Hivyo basi badala ya kuwaza
kutaka kuwa kama fulani, tafakari nini wewe kama wewe unaweza kufanya,
kiwango gani cha uvumilivu na juhudi kinahitajika ili kufikia malengo
yako, na jitahidi kufanya unayotakiwa kufanya kwa juhudi.
Hakuna 'shortcuts' za mafanikio. Na mafanikio ya 'kulazimisha' hayawezi kukuletea furaha ya kweli maishani mwako.
Utakuja kugundua kuwa la msingi sana katika maisha ni kuwa na furaha na amani ya moyoni.
HITIMISHO
Kujitambua mapungufu yako na kuyarekebisha , halafu ukatambua pia mambo
uliyo mzuri sana katika hayo, kisha ukazitumia fursa zinazoendana na
hayo, kutakufanya ujiweke katika namna nzuri ya kupata dili za kuboresha
maisha yako.
Hata hivyo kwakuwa mafanikio ni safari , unapaswa kujipanga kwa kuwa na
taarifa sahihi, kuwa na bidii endelevu katika mambo ya msingi, na zaidi
sana uweze kujitofautisha na wengine ili uweze kutambulika ubora wako,
na hatimaye dili kali zije kwa ajili yako.