Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua
iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake
na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21,
mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika
Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa
mengine hayawezekani kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa
Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa
na Tume na kuegemea katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu
walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na
ubunge kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri
wanatakiwa kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni
pendekezo la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita
mfululizo huku akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa
vimekuwa na mambo mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali
katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema
baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya
chama chake ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu
Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba
Mpya haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo
limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza
kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji
uongozi thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo
la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho
ndicho kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari
masilahi ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.