Dar es Salaam. Watu 56 wamenusurika baada ya ndege ya Shirika la
Ndege la Kenya(Kenya Airways) waliyokuwa wakisafiria kupata ajali
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es
Salaam(JNIA) jana ilipokuwa ikitua.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Kamiishna
Khamis Selemani alithibitisha kutokea kwa ajali akieleza kuwa
ilisababishwa na rubani kupoteza mwelekeo na kushindwa kuona njia sahihi
kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha uwanjani hapo.
Ndege hiyo yenye namba 5Y-FFT aina ya Embrarer 190
yenye uwezo wa kubeba abiria 90 ilipata ajali hiyo mchana ikiwa na
abiria 49 na wafanyakazi saba.
“Tulipata taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo
majira ya saa 8:26 mchana. Ndege hiyo imepata hitilafu katika injini
yake ya upande wa kulia ambayo imebonyea pamoja na kupasuka ubavuni,”
alisema Selemani.
Kamanda huyo aliongeza kuwa pia tairi la mbele la
ndege hiyo limepasuka baada ya kujigonga, lakini hakuna kifo
kilichotokea wala majeruhi waliohitaji matibabu.
“Haitoweza kuruka kabla ya marekebisho kwani hewa
itaingia ndani jambo ambalo haliruhusiwi kwa usafiri wa angani katika
viwango vya kimataifa,” aliongeza Seleman.
Katika hatua nyingine, ndege ya Shirika la Ndege
la Emirates, ilishindwa kutua kwenye uwanja huo jana kutokana na mvua
hizo, hivyo kulazimika kwenda kutua Uwanja wa Ndege wa Mombasa nchini
Kenya.