WAKATI Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
ikiendelea na kikao chake jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Zitto
Kabwe, amekacha.
Zitto ambaye katika siku za hivi karibuni aliibua mjadala kwenye
vyombo vya habari, hasa alipoingia kwenye malumbano na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema, amekacha kikao hicho na badala yake ametoa taarifa
ya kusafiri nje ya nchi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa iliyotolewa kwa wajumbe wa mkutano
huo na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe, ilisema kuwa Zitto
yuko safarini nchini Sudan, lakini anatarajia kuhudhuria mkutano huo
wakati wowote.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kinachofanyika kwenye Hoteli ya
Blue Pearl, jijini Dar es Salaam zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe
wameonyesha dhahiri kukerwa na hatua ya naibu katibu mkuu huyo
kutoshiriki.
Waliolalamikia hatua hiyo walisema kuwa limekuwa jambo la kawaida kwa
Zitto kutohudhuria vikao muhimu vya chama huku akijua fika kwamba yeye
ndiye msaidizi mkuu wa katibu mkuu wa chama taifa.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti hili kuwa moja ya
ajenda zilizowasilishwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi ni kuhusu
mapato na matumizi ya chama ambayo alidai ingefaa Zitto awepo
kuisikiliza.
Mjumbe huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema ajenda hiyo
ilikuwa muhimu kwa Zitto kuwepo kwani akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC), amekuwa akidai kwamba CHADEMA na vyama vingine
hawana hesabu za mapato na matumizi ya fedha za ruzuku wanazopata kila
mwezi.