WIZARA ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imemuumbua Mbunge wa Kuteuliwa, James
Mbatia, kuwa mitihani ya majaribio ya darasa la saba aliyosema ina
makosa ya kisarufi na ilikuwa migumu, ilikuwa feki. Mitihani iliyotajwa
na Mbatia kuwa ina makosa ni ya masomo ya Hisabati, Kiingereza na
Kiswahili na ilifanywa Julai 8-9, 2013 katika wilaya 40 za Tanzania. Taarifa
hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi
katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zuberi Samataba, alipokuwa
akizungumza na MTANZANIA.
“Siyo kweli hata kidogo, mitihani aliyokuwanayo Mbatia ni feki na haikufanywa na wanafunzi wa darasa la saba kama alivyosema.
“Sisi
hatujui Mbatia aliipata wapi hiyo mitihani, halafu wizara haitungi
mitihani bali mitihani inatungwa na NECTA, mitihani ile ilitungwa ikiwa
ni programu maalumu ya kupima uelewa wa wanafunzi wa darasa la saba na
sio moko kama alivyosema.
“Pili ni kwamba, Mbatia alipoiona ile mitihani angefanya jambo la busara
kuwasiliana na sisi kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuzungumza na
vyombo vya habari, kwa sababu tungemueleza ukweli, kwamba mitihani
aliyokuwa nayo ni feki na haijafanywa na wanafunzi wa darasa la saba,”
alisema Samataba.
Alisema kwamba, hata Kamishina wa Elimu wa wizara hiyo, Profesa
Ellustela Bhalalusesa, amelitolea ufafanuzi suala hilo kwamba mitihani
iliyotajwa na Mbatia ilikuwa feki.
“Kamishina kalizungumzia hilo na mimi narudia kulizungumzia, kwamba
mitihani hiyo ilikuwa feki, sasa wewe mtafute Mbatia umuulize mitihani
hiyo aliipata wapi maana iko tofauti kabisa na ile tuliyowapa wanafunzi
wa darasa la saba kuifanya,” alisema.
Majibu hayo, yamekuja ikiwa ni siku chache tangu wizara hiyo izindue
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), katika sekta ya elimu na kujiwekea
mikakati tisa ya kuitekeleza.
Mbatia alipotafutwa ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya mitihani hiyo, hakupatikana.
Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam hivi karibuni, Mbatia
alisema ameibua madudu mapya ya elimu katika mitihani ya Hisabati,
Kiswahili na Kiingereza.
Aliyataja madudu hayo katika mitihani hiyo kuwa, katika Somo la
Kiswahili na Kiingereza, kulikuwa na makosa ya kisarufi wakati katika
Hisabati kulikuwa na maswali yasiyokuwa na majibu.
Alisema aliupeleka mtihani wa Hisabati uliofanywa na wanafunzi hao
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumkabidhi profesa mmoja
(hakutaka kumtaja jina), ambapo aliufanya na kukuta kuna maswali mengine
hayakuwa na majibu kwa sababu yalikosewa.
Aidha, alisema katika mtihani wa Kiingereza na Kiswahili uliokuwa na
makosa makubwa ya kisarufi, aliupeleka katika Jumuiya ya Wanataaluma wa
Chuo Kikuu hicho, ambapo wasomi hao walisikitishwa na makosa yaliyokuwa
katika mitihani hiyo.
Kutokana na madudu hayo, alipendekeza Serikali iunde Tume ya Kudumu ya
Elimu itakayokuwa na hadidu za rejea 12, mojawapo ikiwa ni kushughulikia
ubora wa elimu na kudhibiti mambo yote yanayosababisha kutetereka kwa
ubora huo.
habari NA DENNIS LUAMBANO, DAR ES SALAAM
chanzo - mtanzania