Kampuni kubwa ya teknolojia ya Samsung imepata pigo kubwa la hasara kutokana na hitilafu za simu zake za Galaxy Note 7.
Siku chache zilizopita, kampuni hiyo ilitangaza kusitisha uzalishaji na mauzo ya Galaxy Note 7 kutokana na kesi kadhaa za milipuko ya betri zake zilizoripotiwa na wateja.
Kufuatia uamuzi huo, wataalamu wa kiuchumi wametoa maelezo na kutathmini hasara ya fedha zaidi ya dola bilioni 17 inayoweza kuikumba Samsung kutokana na kuzorota kwa soko la Galaxy Note 7.
Tangu kuingizwa sokoni kwa simu za Galaxy Note 7, kampuni ya Samsung imepokea kesi 92 za milipuko ya betri kutoka Marekani.
Isitoshe, kampuni hiyo pia inakabiliwa na mashtaka kutoka kwa wateja wawili wa Marekani wanaodai kulipwa fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa na milipuko ya betri za Galaxy Note 7.