KAMBI Rasmi ya Upinzani bungeni, jana imeibua tuhuma nzito bungeni Mjini Dodoma dhidi ya Kampuni ya Simu nchini (TTCL), ikidai aliyekuwa Meneja Biashara wa kampuni hiyo (bila kutajwa jina), amefungua akaunti nchini yenye kiasi cha sh. bilioni moja.
Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. Habib Mnyaa (CUF), aliyasema hayo wakati akisoma hotuba ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio, matumizi ya fedha kwa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa, tuhuma hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema ubadhirifu wa fedha kwenye taasisi mbalimbali za Serikali imeota mizizi ambapo baadhi ya watumishi wameamua kujilipa mafao ya kustaafu na kujiongezea mikataba ya ajira.
Aliongeza kuwa, vitendo vya aina hiyo ndio vinavyoendelea katika kampuni ya TTCL vikipata baraka za Wizara husika ambapo baadhi ya watumishi wake wanajinufaisha.
"Mbali ya ufisadi huu, iweje hisa asilimia 35 za Serikali zilizopo ndani ya TTCL zikodishwe kwa Kampuni ya Mobile System International (MSI) kwa kulipiwa sh. bilioni 111 sawa na hisa asilimia 17 lakini Serikali imewapa kuongoza kampuni na hawakulipa pesa yoyote," alihoji.
Bw. Mnyaa alisema hisa zinauzwa na kununuliwa lakini cha ajabu, zimekodishwa kwa anayedaiwa kuwa mwekezaji jambo ambalo ni maajabu kwa tasnia nzima ya uchumi na uhasibu.
Aliongeza kuwa, Kamati ya Wafanyakazi wa TTCL iliandika barua kwa CAG aweze kwenda kufanya ukaguzi maalumu na kuandika barua nyingine kwa Ofisi ya Bunge kuelezea hujuma zinavyofanywa na watendaji waandamizi wa kampuni.
"Ndani ya TTCL kuna umiliki wa SEACOM lakini licha ya Serikali kulijua hilo, bado wanailipa MSI sh. bilioni 14.9, tunamtaka Waziri mwenye dhamana atoe majibu na maelezo ya kutosha juu ya suala hili," alisema Bw. Mnyaa.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wameitaka Serikali kuhakikisha kampuni za simu za mkononi haziwaibii wananchi.
Wakichangia bajeti ya Wizara hiyo, wabunge hao walitaka kujua kama sheria za mitandao ya simu zinabadilika kila mwaka wakidai baadhi ya kampuni za simu zinawaibia wateja wao ambao wengi wao ni maskini jambo ambalo halikubaliki.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, mkoani Mara, Ester Midimu (CCM), alisema inashangaza kuona baadhi ya kampuni hizo zinawakata fedha wateja wao hata kama hawajajiunga na huduma wanazotoa.
"Tulikuwa tunanunua baadhi ya vifurushi kwa sh. 2,800 na kupata dakika zaidi ya 100 lakini hivi sasa tunapata dakika 80, swali langu kila mwaka sheria zinabadilika au la?" Alihoji.
Mbunge wa Chalinze, mkoani Pwani, Bw. Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema hivi sasa baadhi ya kampuni hizo zinawaibia wananchi na kusisitiza kuwa, wizi huo ni mkubwa.
"Tunataka ufafanuzi mzuri juu ya hili kwani ukiweka fedha katika simu inaisha haraka, huu ni wizi mkubwa," alisema.
Kwa upande wake, akiwasilisha makadirio ya bajeti yake, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, aliliomba Bunge lipitishe sh. bilioni 66.9 kwa mwaka wa fedha 2015/16.