SIMBA imempa wiki moja kocha, Goran Kopunovic, awe ametoa jibu kama ataendelea kuifundisha timu yao au ataangalia mipango yake kama alivyowaambia kuwa amekuwa akipokea ofa nyingi ikiwamo ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, hata kabla hajatoa uamuzi wake, viongozi wameanza kufanya michakato mipya ya kuzungumza na kocha wao wa zamani Milovan Cirkovic aliyedaiwa kuwa hana tatizo la kurejea kuifundisha Simba.
Goran amerudi kwao ingawa uwezekano wa kuendelea na Simba ni mdogo kutokana na kuweka masharti makubwa ambayo vigogo wa Simba wameyashindwa na hawakuwa tayari kuendelea kumbembeleza.
Goran amewaambia viongozi wa Simba kwamba Azam wamempa ofa ya maana, lakini cha msingi zaidi ni kwamba hawezi kuzidiwa thamani na wachezaji anaowafundisha na kuwa kama hilo haliwezekani ataondoka, ingawa wameshamseti Milovan tangu juzi na amewaambia dakika yoyote wakiwa freshi wamtumie tiketi aje Bongo kufanya mambo.
Katika masharti aliyotoa Goran, alitaka apewe Dola 50,000 (Sh97.5 milioni) za usajili, mshahara apewe Dola 7,500 (Sh14.6 milioni) kwa mwezi, nauli ya familia Dola 4,704 (Sh9.1 milioni) na alijihakikisha kutwaa ubingwa msimu ujao na kuwataka akitwaa ubingwa apewe Dola 20,000 (Sh39 milioni), mgawo wa getini uwe mkubwa kulingana na mechi pamoja na kuongezwa kwa posho yake.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Simba, zinaeleza kwamba Goran alikuwa hafurahishwi na mambo yaliyokuwa yakiendelea kwenye benchi la ufundi ambayo aliyadai kuwa ni kumwingilia kazi yake.
“Masharti aliyoyatoa ni magumu mno na hakuna kiongozi wa kumbembeleza na sasa tumeanza mipango ya kumrudisha Milovan, tumemwambia afikirie juu ya uamuzi wake wa kuwepo Simba ndani ya wiki moja, ila hatuna mpango naye tena maana anaonekana ni mtu mwenye tamaa,” alisema bosi mmoja wa Simba.
“Kulikuwepo na tofauti kati yake na mratibu wa timu kwani mratibu alitaka mambo yafanyike kwa kuzingatia matakwa ya timu ikiwemo kuwapa mazoezi ya nguvu ambayo yataisaidia timu kufanya vizuri kwenye mechi jambo ambalo yeye hakuwa tayari kulifanya, hapo alionekana anaingiliwa majukumu yake.
“Mratibu aliandika ripoti kwa viongozi juu ya mazoezi wanayopewa wachezaji kuwa hayatoshi kuifanya Simba ishinde na ndiyo maana tulikuwa tunapata matokeo kama yale, leo tunashinda siku nyingine tunafungwa ndipo anashtuka, viongozi walikubaliana na ripoti hiyo ya mratibu.”
Kuhusu usajili ndani ya klabu hiyo, kiongozi huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa mpaka sasa wanaendelea kupokea mapendekezo ya majina ya wachezaji ambao wapo kwenye mpango wa kuwasajili .
“Kocha alitoa mapendekezo yake katika ripoti kwa ajili ya usajili ujao, hivyo tutatumia mapendekezo hayo kwani hatutaki kuangalia sana nje kutokana kwamba hakuna mashindano ya kimataifa tunayoshiriki labda wakati wa usajili wa dirisha dogo tukijua mwelekeo wetu ukoje kwenye ligi.
“Tutaangalia nafasi muhimu kwani sasa tuna wachezaji wanne wa kigeni; Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Simon Sserunkuma na Raphael Kiongera,” alisema.
Kiongera afuatiliwa
Mshambuliaji Raphael Kiongera ambaye anacheza kwa mkopo katika timu yake ya zamani ya KCB ya Kenya ameanza kufuatiliwa mwenendo wake katika mechi anazocheza akiwa na timu hiyo baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi. Kiongera alifanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa mwaka jana.
Hata hivyo, imeelezwa endapo Kiongera atashindwa kurudi katika kiwango chake, anaweza kuachwa.
Kuhusu winga Simon Sserunkuma, imeelezwa alikuwa na tatizo la kisaikolojia na uongozi umeahidi kulitatua ili apige soka.