Header ads

Header ads
» » Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Mstaafu, Jaji Mark Bomani Ataka Kura Ya Maoni ya Katiba Mpya Isogezwe Mbele, Tuendelee na Katiba ya Zamani Kuepusha Machafuko



Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, Jaji Mark Bomani, ambaye pia ni mtaalam nguli wa Katiba, ameonya kuwa iwapo upigaji wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa utalazimishwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, wakati dalili zote zinaonyesha kuwa haiwezekani, unaweza kuzua mtafaruku mkubwa nchini.

Ili kuepusha hali hiyo, ameshauri kura ya maoni iahirishwe hadi baadaye, badala yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iendelee na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa ajili ya kutumika katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Pia, amependekeza kuwa Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977 iboreshwe kwa kuingiza ndani yake mambo mbalimbali, akiwamo mgombea binafsi. 

Jaji Bomani ambaye ni mtaalam nguli wa Katiba aliyewahi kuandika katiba za nchi mbalimbali, zikiwamo za Namibia na Burundi, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete, ya kuipatia Tanzania Katiba mpya, iliharibika baada ya kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba (BMK).
 
Jaji Bomani alisema hilo lilidhihirika baada ya baadhi ya wajumbe wa BMK kujitoa katika Bunge hilo.

“Hili lilikuwa doa kubwa sana kwa mchakato wote. Ilikuwa ni mwanzo mbaya,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza: “Kazi yake (BMK) haikuwa nzuri, haikuridhisha, kwani iliwagawa watu.”

Alisema licha ya baadhi ya wajumbe wa BMK kubaki kwenye Bunge hilo na kuendelea na mchakato hadi kutoa Katiba inayopendekezwa, bado anaona kuna matatizo mawili.

La kwanza, alisema ni kuwapo baadhi ya makundi na watu wanaoamini kuwa Katiba inayopendekezwa imetupilia mbali baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaliyotokana na maoni ya wananchi, hivyo wanaipinga na baadhi yao wanatishia kutoipitisha.

“Hili ni jambo la kusikitisha, lakini siyo jambo la kupuuza. Katiba siyo kitu kinachotegemea kura, bali inatakiwa iwe na muafaka. Kitu hicho Katiba za Namibia na Burundi inacho,” alisema Jaji Bomani.

Alisema katiba ya nchi ndiyo sheria mama na msingi wa kuendesha nchi na kwamba uzuri wake, sharti  uungwe mkono na wengi.
 
Alisema Katiba inayopingwa na kundi kubwa la watu, ni chanzo cha mfarakano kwenye nchi.

Alisema endapo katiba ya namna hiyo inapigiwa kura nyingi za `hapana' au inapingwa na upande mmojawapo wa Muungano iwe Zanzibar au Tanganyika, basi hatima yake ni kuvunja Muungano na kuhoji: “Je, ni sawa tufike huko?”

La pili, alisema ana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kura hiyo kupigwa Aprili 30, mwaka huu, kwani hadi kufikia jana uandikishaji wa wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura ulikuwa ukisuasua.

“Naambiwa eti mpaka sasa waliokwishaandikishwa hawazidi hata milioni moja. Hapo takriban zaidi ya milioni 20 wataandikishwa katika wiki nne zilizobaki? Nafikiri itakuwa ni muujiza kufanya hivyo,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza: “Sasa tufanyeje? Tuendelee na kura ya maoni ambayo ni idadi ndogo ya wapigakura walioandikishwa ndiyo watakaoshiriki, tena kwa suala zito kama la Katiba? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya kosa kubwa sana ambalo litatuletea mgogoro mkubwa na manung’uniko mengi sana nchini. Hivi kweli tufike hapo?”

“Mapendekezo yangu ni kwamba kura ya maoni juu ya Katiba mpya iahirishwe mpaka baaadaye. Badala yake Tume ya Uchaguzi iendelee na uboreshaji wa daftari la wapigakura tayari kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2015. Ikiwezekana hata tuachane na mfumo wa BVR (mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric Voters Registartion), ambao umewapa shida hata wenzetu Kenya na Nigeria.”

Hata hivyo, alisema kwenye rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Katiba inayopendekezwa, kuna mambo mazuri, hivyo akashauri yafanyiwe mabadiliko katika iliyopo ili yatumike kwenye uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na uwakilishi sawa wa jinsia, mgombea binafsi, mgombea urais kupata asilimia 50 au zaidi ili ashinde na Tume Huru ya Uchaguzi.

“Katiba iliyopo inaweza kufanyiwa mabadiliko haraka haraka, tuseme kwenye kikao kijacho cha Bunge tayari kwa matumizi ya uchaguzi mkuu ujao. Litakuwa ni jambo la kusikitisha kuwa hata yale mazuri yasiyo na ubishi yasitumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema Jaji Bomani.

Aliongeza: “Unahitajika muda zaidi wa mazungumzo. Kwani Watanzania tunataka nini au Mtanzania wa kawaida anataka nini? Anataka maisha yake yaboreke, hawataki Muungano wa serikali mbili, tatu wala moja, hivyo ni vitu vya uongozi, havitakiwi uhasama.”

Alisema kura ya maoni haiwezekani kufanyika Aprili 30, mwaka huu kwa kuwa maandalizi hayajafanyika ya kutosha, kwani wapigakura kati ya milioni 20 hadi 23 wanaotarajiwa wanatakiwa wote wapewe nafasi ya kupiga kura.

“Ukiangalia kwenye maandalizi, hatujafika hata nusu. Nina wasiwasi kama hiyo tarehe 30 itafika wote watakuwa wameandikishwa. Tulipe muda. Tusijiongeze kitu kitakachoongeza mfarakano,” alisema Jaji Bomani.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post