Header ads

Header ads
» » Katiba Mpya yabaki kuwa stori

 
Bado hakuna mwafaka kuhusu hatima ya Katiba Mpya, baada ya kuahirishwa kwa upigaji Kura ya Maoni iliyopaswa ifanyike Aprili 30 mwaka huu.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisema Kura ya Maoni itafanyika wakati wowote mwaka huu baada ya kukamilika uandikishaji wapigakura kwa Mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR), wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani, wanaamini kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, kungetoa fursa ya mchakato huo kurudi kwenye Bunge la Katiba.
Wapinzani hao wanasema hili litasaidia kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa Bunge la Katiba ambako kundi hilo lilisusa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, wapo wanaoamini pia kuwa kuahirishwa kwa Kura ya Maoni, ndiyo mwisho wa Mchakato wa Katiba Mpya, hasa baada ya rais aliyeanzisha mchakato huo kumaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu.
Nec iliahirisha Kura ya Maoni iliyopaswa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kutokana na kulegalega kwa shughuli ya kuandikisha wapigakura kwa BVR na baada ya tamko hilo giza likagubika hatima ya mchakato mzima.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na mabadiliko yake yaliyofanyika mwaka 2012 na Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, ziko kimya juu ya nini kinafuata baada ya kuahirishwa kwa Kura ya Maoni.
Sheria hizo zimeeleza tu namna Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unavyopaswa kuendeshwa kuanzia siku ulipotangazwa hadi kupatikana kwa Katiba Mpya. Pia sheria zimeeleza nini kitafuata kama kura ya NDIYO haitafika zaidi ya 50 kutoka pande zote za Muungano.
Kifungu cha 35(3) cha Sheria ya Kura ya Maoni na Kifungu cha 36(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba vinasema kama kura za ndiyo hazifiki zaidi ya nusu ya wapigakura wote Bara na Zanzibar, Tume ya Uchaguzi Nec, na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa makubaliano maalumu na baada ya tangazo la Serikali, watachagua njia nyingine ndani ya siku 30 tangu kutangazwa kwa matokeo hayo.
Ikifikia hapo mchakato wa upigaji Kura ya Maoni utaanza upya. Sheria zote zimempa Rais mamlaka ya kuitisha tena Bunge la Katiba kubadili vipengele vilivyokataliwa wakati wa upigaji kura.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria ya Kura ya Maoni pamoa ja na Kifungu cha  36(5) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vinasema, kama kura za HAPANA zitakuwa nyingi ikilinganishwa na kura ya NDIYO, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.
Vyama vya upinzani kupitia Umoja wao wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamekuwa wakitaka Kura ya Maoni iahirishwe ili kukaa na kutafuta kwanza mwafaka katika baadhi ya mambo ikiwamo Muundo wa Muungano.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa Ibrahim Lipumba, amesema siyo sahihi kuendelea na mchakato wa Kura ya Maoni, kabla ya kupitia upya maeneo yaliyoleta mpasuko kwenye Mchakato wa Katiba.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post