Header ads

Header ads
» » Kanisa ambalo waumini huabudu wakiwa uchi lafungwa

 
WAKAZI wa Ekalakala, eneo la Masinga, Kaunti ya Machakos, mapema wiki hii wakishirikiana na polisi walilifunga kanisa moja eneo hilo kwa madai kuwa waumini wake wanaabudu wakiwa uchi.
Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Masinga, Bw Muraya Mwangi, alisema amekuwa akipokea malalamishi kutoka kwa umma kuwa wanawake wanaohudhuria ibada katika kanisa hilo hutakiwa kuvua nguo wakiombewa.
Bw Mwangi alisema kanisa hilo la Healing Ministry ni la wanawake pekee na kwamba halina ratiba au saa mahususi za ibada.
“Baadhi ya wanawake walipatikana wakiwa uchi ndani ya kanisa hilo chifu wa eneo hilo alipolivamia akiandamana na wakazi,” akasema Bw Muraya.
Afisa huyo aliongeza kuwa kasisi wa kanisa hilo, Joseph Wambua, amekuwa akiongoza kanisa kinyume cha sheria kwa sababu hana stakabadhi zinazohitajika.
Mwenyekiti wa muungano wa wafanyabiashara wa kituo cha biashara cha Ekalakala, Bw Duncan Mutua, alithibitisha hayo na kusema shughuli za kanisa hilo zimekuwa zikifuatiliwa kwa makini baada ya wakazi kulalamikia kuwa linaendesha 'ibada chafu.’
“Kasisi wa kanisa hilo amepatikana mara kadha akiwaombea wanawake wakiwa uchi wa mnyama ndani ya kanisa na hatimaye hatua imechukuliwa,” akasema Bw Mutua.
Aliongeza kuwa wasiwasi kuhusu shughuli za kanisa hilo uliongezeka baada ya wanawake wa eneo hilo kutumia muda wao mwingi kanisani na hata kuacha waume wao usiku kwenda kwa ibada za 'kesha.’
“Tulivamia kanisa hilo na kumfumania kasisi akiwamwagilia wanawake maji wakiwa uchi wa mnyama. Alijitetea akisema alikuwa akiwafanyia maombi spesheli,” akasema.
Alisema baadhi ya wanawake ambao ni waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakizozana na wanaume wao tangu kanisa hilo lifungwe.
Kuhubiri injili
Lakini Kasisi Wambua alikanusha madai hayo na kuyataja kuwa ya uwongo akisema kanisa lake limekuwa likihubiri injili eneo hilo kwa 'njia zinazofaa’ na kuwalaumu maafisa wa utawala wa eneo hilo kwa kudai hongo kutoka kwa kanisa hilo kila mwezi. “Shida hizi zote zimesababishwa na machifu wa eneo hili ambao wamekuwa wakidai hongo kutoka kwangu,” akasema Bw Wambua.
“Hili ni kanisa linalomcha Mungu na madai haya yote hayana msingi wowote,” akaongeza. Maafisa wa polisi walisema kanisa hilo litafungwa hadi uchunguzi kuhusu shughuli zake ukamilike.
Wakazi wa Masinga wanasema kanisa hilo lilivutia waumini wengi kutoka kanisa la Africa Inland Church (AIC) ambalo lina wafuasi wengi kutoka eneo hilo. “Lilianzishwa mwaka uliopita na baada ya miezi sita lilikuwa limevutia zaidi ya waumini 100 wengi kutoka AIC,” akasema mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Inasemekana Bw Wambua aliripoti kufungwa kwa kanisa lake kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Masinga ambaye aliagiza machifu wafike afisini mwake jana.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post