Header ads

Header ads
» » TAARIFA KAMILI::BINTI WA PROFESA AUAWA KWA SUMU

Stori: Deogratius Mongela na Chande Abdallah
WAKATI Wakristo kote nchini wakijiandaa kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, keshokutwa Alhamisi, baadhi ya familia zipo kwenye majonzi mazito kufuatia kuondokewa na ndugu zao, Uwazi lina kisa cha kuumiza.
Marehemu Neema Malimbwi enzi za uhai wake.
Jijini Dar es Salaam, binti mbichi aliyejulikana kwa jina la Neema Malimbwi (pichani) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Kodi Tanzania (ITA) ambacho kipo chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  kilichopo Mikocheni jijini Dar amefariki dunia kwa madai ya kulishwa sumu kwenye kinywaji.
Marehemu Neema alikuwa binti wa  profesa wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (Sua), Rogers Malimbwi.
SIKU YA TUKIO
Tukio hilo la kusikitisha linatajwa kutokea usiku wa Alhamisi,  Desemba 18, mwaka huu wakati Neema anarudi hosteli maeneo ya Kijitonyama, Dar ambapo alikuwa akiishi.
ALIKWENDA KUJIRUSHA B BAND
Kwa mujibu wa chanzo chetu, siku ya tukio, Neema alikuwa na marafiki zake wavulana kwa wasichana kwenye onesho la muziki wa B Band inayomilikiwa na Banana Zorro ambapo akiwa huko saa 7 usiku aliendelea kuchati na marafiki zake waliokuwa hosteli akitumia ukurasa wake wa Facebook akiwaambia kuwa alikuwa ‘kiwanja’ akiponda raha.
Baba wa marehemu Neema Malimbwi, Prof. Rogers Malimbwi.
Habari zinadai kuwa, marehemu Neema usiku huo alikuwa akihama maeneo mbalimbali akiwa na vijana ambao baadhi ya marafiki zake wanadai huenda walihusika na kumtilia sumu kwenye bia alizokuwa akinywa.
MATATIZO YALIPOANZA
Habari zaidi zinasema kuwa, Neema akiwa na wenzake wakirudi hosteli, njiani alianza kulalamikia kutojisikia vizuri.
“Alikuwa njiani na wenzake wakirudi kulala, akaanza kulalamika kwamba hajisikii sawasawa, ikabidi wenzake wamkimbize Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu wa Kinondoni, Palestina, Sinza, Dar ambako waliambiwa kuwa kutokana na hali yake kuwa mbaya wampeleke kwanza Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar ili kupata hati ya matibabu (PF3),” kilisema chanzo kimoja.Chanzo hicho kikaendelea kudai kwamba, walipofika Mabatini waliambiwa waende Kituo cha Polisi Oysterbay.
AKIMBIZWA HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Ikazidi kudaiwa kuwa, Polisi Oysterbay walitoa msaada kwa haraka ambapo sasa ikabidi Neema akimbizwe Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu Kinondoni, Mwananyamala ambako alifariki dunia.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura (aliyesimama) akizungumza jambo.
ALIJITABIRIA KIFO
Chanzo hicho kilisema kuwa, denti huyo alikuwa kama anafahamu siku ya kifo chake ambapo siku moja kabla alimshukuru Mungu kupitia ukurasa wake wa Facebook kwa yote aliyomfanyia kisha kutuma picha mbalimbali akiwa katika pozi tofauti.
MWILI WAKE MOCHWARI
Mwili wa Neema ulihifadhiwa kwenye mochwari ya Mwananyamala kabla ya kusafirishwa juzi kwenda Morogoro kwa mazishi yaliyofanyika jana.
KUMBUKUMBU MBAYA
Kumbukumbu zilizopo kwenye makabrasha ya gazeti hili zinaonesha kuwa, Juni Mosi, mwaka jana, mama mzazi wa Neema, Elizabeth Malimbwi alifariki dunia kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar na mwili wake kwenda kuzikwa Morogoro.
Tangu kifo cha mama yake, baadhi ya madenti wenzake wanasema, Neema amekuwa akiishi maisha ya mawazo sana na muda mwingi alikuwa akiutumia kunywa pombe kiasi kwamba, darasani ilikuwa mara chache sana kuhudhuria.
Neema Malimbwi enzi za uhai wake akiwa hosteli.
RPC ATHIBITISHA KIFO
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura alikiri kuwa na taarifa hizo.“Ni kweli taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo ninazo,  mpaka sasa jeshi la polisi linasubiri ripoti kamili ya uchunguzi wa madaktari kuhusiana na kifo chake,” alisema Kamanda Wambura.

CHANZO CHA HABARI
GLOBAL PUBLISHERS

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post