LICHA ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kukanusha mara zote kwamba, hahusiki na kusambaratika kwa ndoa ya Mwimba Injili Flora Mbasha na mumewe, Emmanuel Mbasha, lakini mume huyo ambaye amekuwa akimshutumu Gwajima ameibuka na jipya, Amani linakupa zaidi.Mwimba Injili Flora Mbasha na mumewe, Emmanuel Mbasha
Jipya aliloibuka nalo Mbasha ni kudai kuwa, msala uliompata Mchungaji Gwajima wa kumtolea maneno yenye kuudhi Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kadinali Pendo na kisha kuhojiwa polisi na kupata mshtuko, kuzimia hadi kulazwa hospitali ni malipo ya Mungu kwake kutokana na kilio chake.
ATUMIA DAKIKA 15
Akizungumza na Amani kwa njia ya simu kwa dakika 15 juzi, Mbasha alisema: “Ile hali (kupoteza fahamu) ya Gwajima ni malipo. Mimi nilishasema jamani, mtu akikutendea ubaya malipo ni hapahapa duniani, hakuna kwingine.
“Mimi ndoa yangu haipo, mke wangu anajua yeye anavyoishi. Kwa hivyo mimi nimekuwa nikiishi kwa manung’uniko kila siku, unadhani nini kitatokea kwake?”
AMTAKA AKAMWOMBE MSAMAHA
Mbasha alikwenda mbele zaidi kwa kutoa tamko na agizo kwa mchungaji huyo kwa kusema:
“Tena namwomba Mungu ampe afya Gwajima, akitoka hospitali alikolazwa (TMJ, Dar) anitafute kuniomba msamaha.
“Ni vyema na itakuwa vyema zaidi akinitafuta na kuniomba msamaha ili kila mmoja aishi kwa amani. Mimi nisiwe na kinyongo na yeye na wala yeye asiwe na kinyongo na mimi.”
KUHUSU ALICHOKIONGEA GWAJIMA
Mbasha hakumalizia hapo, alipoulizwa kama kauli ya Gwajima iliyosababisha mtafaruku ilikuwa sawasawa au la! Mbasha alisema:
“Hilo atajua yeye mwenyewe na Mungu wake, mimi sijui. Ila ninachojua mimi ni kitu kimoja tu, kwamba Mungu amenilipia basi, sasa aniombe msamaha.”
MCHUNGAJI WA GWAJIMA ANENA
Naye mchungaji mmoja wa kanisa la Gwajima alipopatikana kwa simu na kuulizwa kuhusu madai ya Mbasha, alisema: “Yule hajui maandiko sawasawa. Hakuna uhusiano wowote kati ya kilichompata mchungaji wangu na hisia zake kuhusu mkewe Flora.
“Gwajima na Flora hawana uhusiano wowote usiofaa. Sasa yeye anaposema kalipiwa, kalipiwa kitu gani? Mungu anaweza kulipa jambo la hisia?”
WANACHOAMINI WENGINE
Mbali na Mbasha, baadhi ya wasomaji wa gazeti hili walisema kwamba, wanamwamini Mchungaji Gwajima ni miongoni mwa watumishi wa Mungu waliojaliwa hekima hivyo kauli aliyoitoa yenye maneno yenye kuudhi huenda ulikuwa mpango maalum wa roho chafu aseme yale ili yamkute yaliyomkuta na kujifunza kitu.
“Gwajima ana hekima bwana. Ni Mchungaji mwenye kujitambua, yale maneno aliyomsema Askofu Pengo lazima ni mpango wa roho chafu, pale Gwajima ana kitu cha kujifunza.
“Mimi sisemi kama alichokutananacho ni kwa sababu ya ‘maombi’ ya Mbasha kwa Mungu wake, ila nasema Gwajima ana kitu cha kujifunza kwa matamshi yake na mazingira ya utumishi pia,” alisema Johnson Mwaduma, mkazi wa Mwananyamala, Dar.
WITO KWA SERIKALI
Kufuatia manenomaneno ya chini kwa chini kwamba, huenda serikali ikalifungia kanisa lake lililopo Kawe jijini Dar, baadhi ya wasomaji waliitaka serikali kutofikiria kufanya hivyo kwani Gwajima ni mchungaji mwenye waumini wengi sana nchini.
“Yule ana makanisa nchi nzima, sasa serikali ikisema ilifungie kanisa lake ina maana waumini maelfu kwa maelfu watarudi nyuma kiroho na matokeo yake ni kuanza kupata watu watenda maovu.
“Lazima ikumbukwe kwamba, mchungaji anapowahubiria waumini wake kutenda mema, kuacha dhambi pia anaisaidia serikali katika kupambana na maovu.
“Halafu yule Gwajima mwenyewe ni mchungaji wa kweli, ana imani, ana nguvu ya kiroho, amesaidia wengi kimwili na kiroho pia. Anatakiwa kuendelea kutiwa moyo kwa vile ni mtu mwongofu,” alisema Simon Salele, mkazi wa Sinza D, Dar es Salaam.
TUJIKUMBUSHE
Wiki mbili zilizopita, kwenye Viwanja vya Tanganyika Perkers ambako kuna kanisa, Gwajima alitoa mahubiri yaliyolenga kumshutumu Kadinali Pengo kwa kitendo chake cha kwenda kinyume na maazimio ya Baraza la Maaskofu Tanzania kuhusu msimamo wao wa Mahakama ya Kadhi nchini.
Hali hiyo ilimfanya Gwajima kuitwa Polisi Kituo cha Kati, Dar na kuhojiwa. Akiwa katika mahojiano, ghafla alisikia kizunguzungu, akaanguka na kupoteza fahamu. alikimbizwa katika Hospitali ya Polisi Baracks kisha Hospitali ya TMJ, Dar kwa matibabu zaidi.
Juzi, Gwajima aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo lakini akachukuliwa hadi Kituo cha Polisi Oysterbay kwa mahojiano zaidi na kuachiwa kwa dhamana.