Homa
ya uchaguzi inazidi kupanda kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge
na rais unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu huku habari kubwa
ikiwa ni jeuri ya fedha iliyooneshwa na chama kipya cha Zitto Kabwe,
Alliance for Change and Transparency (ACT- Tanzania) kufanya uzinduzi wa
kihistoria uliogharimu mamilioni ya fedha.
Mh. Zitto Kabwe
Zitto
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), alitimuliwa kwenye chama hicho hivi karibuni na
siku chache baadaye, akaibukia kwenye chama hicho na kuchaguliwa kuwa
Kiongozi Mkuu Taifa wa chama hicho.
Baada
ya uchaguzi huo, Machi 29, 2015, ACT kilizinduliwa rasmi katika hafla
kubwa iliyoacha gumzo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee
jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha watu mbalimbali kutoka mikoa
kadhaa ya Tanzania sambamba na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi.
Jeuri
ya fedha iliyotumika kwenye uchaguzi huo, kwa kukodi ukumbi wa gharama,
kuwagharamia wajumbe wote kutoka mikoani na kurusha matangazo ya
runinga moja kwa moja kupitia runinga za ITV na Azam TV, ilisababisha
minong’ono mingi kuanza kusambaa kwamba nyuma ya chama hicho, kulikuwa
na mkono wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Haiwezekani
chama ndiyo kwanza kimeanzishwa juzijuzi tu halafu wawe na jeuri ya
fedha kiasi hiki, kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye runinga
mbili za ITV na Azam TV kunagharimu fedha nyingi sana, Zitto na wenzake
wamepata wapi fedha hizo? Kuna mkono wa mtu hapa,” mdau mmoja aliyeomba
hifadhi ya jina lake, aliliambia Uwazi Mizengwe nje ya ukumbi huo wakati
uzinduzi ukiendelea.
Wasomaji
wengine waliofuatilia uzinduzi huo, walipiga simu chumba cha habari na
kudai kuwa kuna zengwe limeandaliwa kumpaisha Zitto na chama chake kwa
lengo la kupunguza kura za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika
uchaguzi mkuu ujao.
“Hawa
jamaa (CCM) ni wajanja sana, wameamua kuwekeza ACT kwa kuwapa fedha na
kuwagharamia kila kitu ili kuwachanganya wapinzani. Unajua mpaka sasa
tayari kuna watu walikuwa Ukawa wameshahamia kwa Zitto, CCM wamefanya
makusudi ili waendelee kutawala, wanatumia ile falsafa isemayo ‘Divide
and Rule’ (Gawanya kisha Tawala),” alisema Sunday Makweta wakati
akizungumza na gazeti hili.
Ili
kupata ukweli wa zengwe hilo, Uwazi Mizengwe liliingia kazini ambapo
lilianza kwa kumtafuta Zitto. Alipopatikana, alisomewa madai kwamba
chama chake kinadaiwa kufadhiliwa na CCM kwa lengo la kudhoofisha Ukawa
ambapo alishangaa madai hayo na kufunguka:
“Huyo
anayetuhumu hivyo aseme huyo mfadhili ni nani na kafadhili nini. Yeyote
mwenye mawazo hayo hafikirii. Wanachama wamejitolea, gharama za kurusha
matangazo ya moja kwa moja tumepewa discounts (punguzo la bei).
Tumechanga kutoka kwa marafiki, hiki chama ni sawa na moto wa pumba, ni
chama kikubwa na tumedhamiria.”
Uwazi
Mizengwe lilimtafuta pia mwenyekiti wa chama hicho (Taifa), Annastazia
Mghwira alisema si kweli kwamba chama chao kinafadhiliwa na CCM kwa
sababu kwanza wana kesi dhidi ya chama hicho mahakamani kutokana na
madai ya kuibiwa kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Chama chetu kinapaa kutokana na wanachama kujitolea na tunataka kuhamisha uwezo kwa wananchi na kuing’oa CCM madarakani.”
Baada
ya kusikia kwa upande huo, Uwazi Mizengwe pia lilimtafuta Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na kumuuliza kuhusu madai ya chama
chake kukifadhili ACT kwa lengo la kudhoofisha nguvu za Ukawa ambapo
alikanusha vikali chama chake kuhusika kwa namna yoyote na chama cha
ACT.
“CCM
ni taasisi kubwa yenye wanachama na wapenzi wengi. Huwezi kuihusisha na
chama chochote cha siasa. Najua kuna watakaosema chama cha Zitto ni CCM
B lakini ukweli ni kwamba wanaovumisha hayo ni Ukawa ambao
wamefilisika.
“Ninachoweza
kutabiri kwa sasa ni kwamba mara baada ya kura za maoni kuhusu Katiba
Inayopendekezwa kupigwa, Ukawa itakufa na watasema pia kuna mkono wa CCM
wakati ukweli ni kwamba watakuwa hawana ajenda tena,” alisema Nape.
Aliongeza
kwamba hivi sasa wanashughulika na ukaguzi wa uhai wa chama nchi nzima
na juzi walikuwa wakimalizia ziara yao mkoani Kilimanjaro.
“Hapa
tumefanya vizuri sana na uhai wa chama umeimarika... wapinzani waachane
na kudhani CCM itaacha kazi zake na kushughulika nao, tuna kazi nyingi
za kushughulikia kero za wananchi maana ndiyo wapiga kura wetu na
migogoro yao wasituingize, Zitto amekosana na Chadema siku nyingi na
sisi CCM tulikuwa tukisoma tu kwenye vyombo vya habari,” alisema Nape.
Kwa
upande wa Ukawa, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa,
akizungumzia ujio mpya wa Zitto na hofu ya chama hicho kupunguza kura
zao kwenye uchaguzi mkuu ujao, alifunguka:
“Katika
vitu ambavyo havitunyimi usingizi katika uchaguzi mkuu ujao ni ACT na
Zitto...siyo tishio kwa Ukawa hata kidogo. Hawezi kuipasua Chadema wala
Ukawa na mtakubaliana nami baada ya uchaguzi mkuu kufuatia matokeo
atakayoyapata.”
Naye
Mkuu wa Idara ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk. Benson Bana, akizungumza na waandishi wa habari hivi
karibuni, alisema Ukawa hawapaswi kuipuuza ACT kwani kama itajipanga
vizuri na kuepuka migogoro ya ndani ya chama, inaweza kujizolea kura
nyingi kwenye uchaguzi ujao na hivyo kupunguza nguvu ya Ukawa.
“Zitto
bado ni hai kisiasa, anajua kujenga hoja na akaisimamia mpaka mwisho.
Ana ushawishi mkubwa, anaheshimika, na kupendwa na nchi nzima kwa jumla,
uwepo wake ndani ya ACT wanaweza kupanda chati haraka na kuwa miongoni
mwa vyama vya siasa vyenye wafuasi wengi na vyenye nguvu nchini,” alisema.