Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini
SERIKALI imesema ajira za walimu wapya
zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku ikiweka wazi kuwa walimu hao
wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea
kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na idadi ya walimu waliopo ni
kubwa na inakidhi mahitaji, huku maeneo yaliyopewa kipaumbele ni
vijijini na halmashauri ambazo zina mahitaji na upungufu mkubwa wa
walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira
zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795,
Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne
Sagini wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za
walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo
zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi ya shule ili
kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmahauri na
shule.
“Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa
halmashauri na shule hasa za mjini zenye walimu wa ziada na zingine hasa
za vijijini zina upungufu mkubwa wa walimu,” alisema Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia kuwapanga
walimu wapya kwa usawa ili kuondoa uwiano usioridhisha kwenye maeneo
mengi ya vijijini. Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu za kupata
kibali kwa ajili ya ajira za walimu na fedha za kuwalipa stahili zao ili
waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo
watakavyopangiwa vitawekwa katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
TAMISEMI ambayo ni www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu www.moe. go.tz
ifikapo Aprili 24, mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa
TAMISEMI, Zuberi Samataba alisema, pia ufuatiliaji huo ulikuwa ni
kuhakikisha wanakuwa na taarifa sahihi za walimu wanaoajiri wote ni
wapya ambao hawajawahi kuajiriwa ili kuepuka usumbufu kwa walimu ambao
hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao
wameshaajiriwa wanapoenda kusoma, hupangiwa upya vituo na hawatoi
taarifa hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa kutopata mishahara yao.
“Kuna baadhi ya walimu wameshaajiriwa kwa
hiyo jina linapoingizwa katika taratibu za malipo, linagoma kuingia
ndipo ukifuatilia unajua alikuwa ameajiriwa, inabidi umwambie arudi kwa
mwajiri wake.
Kwa hiyo kwa hawa walimu wapya nawashauri
waende kuripoti katika vituo walivyopangiwa na wakubali kufanya kazi
katika maeneo hayo, sio waripoti halafu waondoke,” alisema.
Wakati huohuo, Serikali imewataka
Makatibu Tawala wa Mikoa ambayo shule zake zimefungwa kwa madai ya
ukosefu wa chakula, kuwachukulia hatua wakuu wa shule hizo, kwa kile
kilichoelezwa kuwa wamekiuka utaratibu kutangaza hivyo ilhali serikali
ilishatuma fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi katika shule
mbalimbali nchini.
Shule zilizofungwa kwa tatizo hilo na
mikoa yake kwenye mabano ni Rugambwa, Kahororo, Nyakato na Ihungo
(Kagera), Lyamungo (Kilimanjaro), Mpwapwa na Abeid Karume (Dodoma),
Kazima, Milambo, Wavulana Tabora na Wasichana Tabora (Tabora).
Uamuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Jumanne Sagini aliyesema serikali imeshatoa asilimia 66.7 ambazo ni Sh
bilioni 28.1 zilizotengwa kwa mwaka 2014/2015.
Alisema serikali imetoa fedha hizo katika
kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu kwa ajili ya
chakula cha wanafunzi wa shule za sekondari, zinazomilikiwa na serikali.
Sagini alisema serikali ilitenga Sh bilioni 42.1 kwa mwaka 2014/2015,
ambapo kati ya fedha hizo kiasi kilichobaki ni Sh bilioni 13.9, sawa na
asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa.
“Kwa ufupi, serikali haijafunga shule na
wakuu wa shule waliotangaza kufunga shule hizo chache wamefanya makosa
kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka husika ili kupata kibali kama
kungekuwa na sababu ya kufanya hivyo, naamini mamlaka husika
zitawachukulia hatua,” alisema Sagini.
Alisema wamiliki wa shule ni Mamlaka za
Serikali za Mitaa, ambazo watendaji wake ni wakurugenzi na wakuu wa
shule ni viongozi wasimamizi wa shule hizo, hivyo hawana mamlaka ya
kutangaza kufunga shule kwa sababu yoyote bila kibali cha mwenye shule.
Kwa mujibu wa Sagini, kuna utaratibu wa
kufunga shule ambapo katika kipindi hiki, shule nyingi zilikuwa
zimefungwa kwa mapumziko mafupi kati ya Machi 28 hadi Aprili 12, ambapo
katika shule hizo zilizofungwa wanafunzi walilazimika kurudi makwao
kutokana na kutangaziwa na wakuu wao wa shule.