Polisi mkoani Tanga imesema imefanikiwa kupata bunduki aina ya SMG, ikiwa na risasi 20 ndani ya mapango ya Majimoto katika eneo la Amboni, inayodaiwa ilikuwa ikitumiwa na wahalifu waliorushiana risasi na askari mwishoni mwa wiki.
Aidha,
imesema inashikilia watu kadhaa akiwemo aliyesababisha kupatikana kwa
bunduki hiyo. Baadhi ya watu wanaendelea kuhojiwa, kupata taarifa kwa
lengo la kukamata waliopora silaha kwa askari na kurushiana risasi
kwenye mapango hayo.
Kupatikana
kwa silaha hiyo, kunafuatia msako maalumu uliodumu kwa siku nne sasa,
uliolenga kusaka silaha na wahalifu wanaodaiwa kujificha ndani ya
mapango ya mawe yaliyopo Amboni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema
mafanikio hayo, yametokana na subira ya wakazi wa Tanga na ushirikiano
mkubwa wanaoendelea kuuonesha kwa Polisi inayoshirikiana na vikosi
vingine vya ulinzi na usalama, kufanya operesheni ya pamoja kwenye eneo
hilo.
“Kutokana
na taarifa kutoka kwa wananchi Februari 16 mwaka huu katika kitongoji
cha la ‘Kona Z’ kilichopo Amboni, tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja
ambaye kwa sasa sitamtaja jina kwa sababu upelelezi unaendelea,
tulimhoji kwa kina akatupa taarifa kuhusu silaha hii,” alisema.
Alieleza, “Tulikwenda
mpaka pangoni na kufanikiwa kupata SMG hii ikiwa na magazini moja na
risasi 20… silaha hii ni miongoni mwa zilizoporwa kwa askari mwezi
uliopita”.
Alisema
licha ya kupatikana kwa silaha hiyo, watu kadhaa wanashikiliwa
wakihusishwa na tukio hilo. Alisema upelelezi unaendelea kupata taarifa
za kuwezesha kupatikana kwa silaha nyingine na vitu mbalimbali
vilivyowahi kuibwa.
“Naomba
wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla muendelee kuvuta subira na
kutoa ushirikiano…endelezeni utulivu na mshikamano kwa jeshi la polisi,
ili kwa pamoja tuweze kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema
upo umuhimu mkubwa kwa wananchi, kuendeleza utulivu kwa kutokubali
kuamini taarifa potofu zenye kujenga hofu, zinazosambazwa na baadhi ya
mitandao ya kijamii kwa kuwa zinalenga kuwavuruga.
“Kimsingi
jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama, linaamini na
kuthamini kazi ya vyombo vya habari hasa vile makini, ambavyo
vimeendelea kuwaarifu wananchi habari sahihi ambazo hazina ghilba wala
kuwachanganya”, alisema.
Alikanusha
taarifa zilizoenea mjini kwamba ipo miili ya wahalifu,iliyokutwa ndani
ya mapango hayo, kutokana na mapigano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Ndugu
zangu mwanzoni tulikuwa tukisikia harufu kali ya kama miili iliyooza,
kweli tulijitahidi kutafuta na tukafanikiwa kuona mizoga ya ngedere na
siyo binadamu ...wanyama hao walikuwa watatu na walikuwa na majeraha
makubwa sana. Kwa hiyo hawakuwa watu, bali ni ngedere ndio walikokuwa
wamekufa na kuoza humo pangoni,” alisema.
Akizungumzia
mkakati wa kupata silaha iliyosalia na vifaa vingine vilivyoporwa,
Chagonja alisema jeshi lake na kikosi cha operesheni hakitalala usingizi
mpaka vitu vyote vipatikane.