Header ads

Header ads
» » Wamasai na wanyama katika Hifadhi ya Ngorongoro ni Zaidi ya Marafiki

 
Licha ya umaarufu wake, Hifadhi ya Taifa Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha ina mambo mengi ya kuvutia yanayoifanya muda wote kuwa ya kipekee duniani.
Upekee huo unatokana na mfumo wa maisha ya binadamu yanavyohusiana moja kwa moja na maisha ya wanyama.
Siyo jambo geni kusikia kuwa binadamu hasa wa jamii ya Kimasai wanaoishi kwenye eneo la hifadhi hiyo wanaishi na mifugo yao katika maeneo yaliyo na wanyamapori bila kudhuriana.
Hata hivyo, jambo linaloweza kuwa geni na la ajabu ni baadhi ya koo za Kimasai ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuelezwa kwamba ‘zina udugu’ na baadhi ya wanyama. 
Licha ya maelfu ya watalii kutembelea hifadhi hiyo ili kufaidi na kuona wanyama waliosheheni Ngorongoro, kasi ya wageni hao pia ni kubwa kutembelea jamii ya Wamasai inayoishi eneo hilo ili kujua mila na tamaduni zao na namna wanavyoweza kuishi na wanyama.
Hakika hakuna ubishi kwamba Wamasai wa Ngorongoro na wanyama katika Hifadhi ya Ngorongoro ni marafiki.
Ukweli huo unakwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa  hata baadhi ya koo za Kimasai, ‘zina udugu’ na wanyama kwa kadri ya majina yao.
Inaelezwa kuwa kuna ukoo wenye ‘udugu’ na nyoka, mwingine simba hata wanyama wengine.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Vincent Mbilika anaeleza kuwa zipo koo ambazo majina yao yana uhusiano na wanyama hata wadudu.
Mfano; ukoo wa Mollel unatajwa kuhusiana na faru, Laitayok unahusiana na tembo na mbogo, nyani na tumbili wanahusianishwa na  ukoo wa Ilukumai, ambao fisi na nyoka wanaelezwa kuwa na uhusiano na ukoo wa  Illtarru-sero.
Mbilika anaeleza kuwa katika koo iliyo ndugu na nyoka, jamii hiyo ikikuta nyoka ndani ya nyumba yao haipambani naye tofauti na ilivyo kwa jamii nyingine, zinachofanya ni humwekea  maziwa kwa kumwagia, naye huyanywa.
“Baada ya kupewa maziwa, hutoa ndimi zake na kulamba maziwa kisha hutoka ndani ya nyumba  bila kudhuru mtu, tena anatokea mlangoni. Hivyo, koo  yenye udugu na nyoka  hata kama ni mkubwa kiasi gani, ikiwa ameingia ndani ya nyumba, hata kufikia hatua ya kulala kitandani na mtoto mdogo, hauawi,” anasema Mbilika.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post